Mchungaji msataafu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Ambilikile Masapile, anaendelea kusakamwa na wagonjwa wanaodai hawakuponeshwa na dawa yake, wapo walioweka nia ya kumburuza mahakamani lakini la kusikitisha zaidi ni kumfilisi. Wanaharakati wameeleza kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo wanamfungulia Babu Ambi, mojawapo ni kumfilisi mali zote alizochuma endapo atakutwa na hatia ya ulaghai, wakati wa kutangaza maono aliyopewa na Mungu kuhusu tiba ya kikombe. Wanadai kuwa Babu Ambi, mkazi wa Kijiji cha Samunge, Loliondo, alitumia matatizo ya Watanzania ya kuugua maradhi sugu ili kujinufaisha, hivyo akatengeneza ulaghai wa tiba ya kikombe kwa maelezo kwamba ni ufunuo aliopewa na Mungu. Madai hayo yanakuja wakati ambao Babu Ambi ameukata, ameshakamilisha ujenzi wa nyumba yake ya kisasa kijijini Samunge, pia anamiliki magari mawili ya bei mbaya, Toyota Land Cruiser (pick-up) na Isuzu (pick-up). Babu Ambi, ameshahama nyumba chakavu aliyokuwa anaishi zamani na sasa anaendesha maisha yake kwenye nyumba mpya ya kisasa ambayo kwa Samunge, inaonekana ni kama Ikulu kwa jinsi inavyomeremeta.
Jamani wasomaji hiyo ndio ikulu wanaharakati na baadhi ya wagonjwa wa Babu wanailalamikia kuwa kawadanganya apate fedha za kujengea.
Wanaharakati wameenda mbali mpaka kubeza kuwa Babu hakustahili kuishi kwenye nyumba ndani vigae mpaka maliwatoni. Mpendwa msomaji hizi ni baadhi ya shutuma zinazomsibu Babu wa kikombe. Ulimwengu una mambo, wako wanaosema Babu kawarusha roho watu kwa manufaa yake binafsi na wako wanaodai kazifanyia kazi hela zilizotokana na uponyaji pia wako waliokaa kimya. Msomaji wewe uko upande gani? Watu walifumbwa macho muda wote ule tangu Babu alipoanza tiba mpaka alipojenga nyumba ndo wanastuka?
No comments:
Post a Comment