Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, mchumba wake Bikira Maria, Msimamizi wa Kanisa, siku kuu inayofanyika kila mwaka tarehe 19 Machi, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsimika rasmi Askofu Salutaris Libena kuwa askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Ifakara ililoundwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ili kusogeza huduma za kichungaji kwa waamini.
Askofu Libena aliwasili Jimboni Ifakara, Jumamosi tarehe 17 Mchi, 2012, na kupokelewa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema. Katika hotuba yake fupi, Askofu Telesphori Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, alimtaka Askofu Libena kusimama kidete kulinda na kutetea imani na mafundisho ya Kanisa, bila kuogopa kwani wapo ndugu zake katika hurika wa uaskofu ambao wako tayari kumsaidia katika maisha na utume wake. Anawaalika Mapadre, watawa na waamini walei kutoa ushirikiano wa dhati kwa Askofu wao ili aweze kutekeleza majukumu yake ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Ifakara. Alipowasili, Askofu Libena na msafara wake wametembelea Parokia za Msolwa, Mkula na Kisawasawa. Jumapili tarehe 18 Machi, Askofu Libena ametembelea makao makuu ya Jimbo Katoliki Ifakara pamoja na Parokia ya Kibaoni. Jumapili jioni, katika Ibada ya Masifu ya Jioni, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, aliikabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu.
Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge amewakumbusha waamini kwamba, kumegwa kwa Jimbo la Mahenge na kuundwa kwa Jimbo Katoliki la Ifakara kunapania kuboresha huduma za kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimboni humo, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni Familia ya Mungu kuonesha ushirikiano wa dhati na Askofu Salutaris Melchior Libena.
No comments:
Post a Comment